28 Mei 2026 - 19:01
Sheikh Prof. Alhad Mussa Salum Atoa Nasaha za Eid al-Adha na Hijja: Ibada Ifanywe kwa Ikhlasi na Si Kujionesha Mitandaoni

Sheikh Profesa Alhad Mussa Salum amesisitiza umuhimu wa uelewa sahihi wa ibada za Eid al-Adha na Hijja. Ameeleza kuwa kondoo ni mnyama bora zaidi kwa kuchinjwa katika Eid al-Adha endapo anapatikana, na hata nyama yake ni bora zaidi Bali Kondoo Ndiye asili ya ibada hiyo. Kuhusu Hijja, amebainisha kuwa ni ibada ya kuitikia wito wa Mwenyezi Mungu kupitia Nabii Ibrahim (as), na huleta utakaso wa dhambi kwa mja. Ameonya baadhi ya mahujaji kukosa maandalizi ya kiroho na kurejea katika dhambi baada ya Hijja. Ameikosoa tabia ya kutumia ibada ya Hijja kwa kujionesha mitandaoni kupitia Picha za “selfie”, akisisitiza kuwa ibada ni kwa ajili ya Mwenyezi Mungu pekee. Amemalizia kwa kusisitiza msingi wa ikhlasi na kuepuka riyaa katika ibada zote.

Kwa Mujibu wa Shirika la Habari la Ahlul-Bayt (as) -ABNA-  Sheikh Profesa Alhad Mussa Salum, Mwenyekiti wa Jumuiya ya Maridhiano na Amani Tanzania (JMAT-TAIFA), ametoa nasaha kuhusu maana na utendaji sahihi wa ibada ya Eid al-Adha na Hijja, akisisitiza umuhimu wa uelewa wa ibada pamoja na uadilifu wa kiroho.

Katika nasaha zake, Sheikh Pro.Alhad amesema kuwa watu wengi huelekea kuchinja mbuzi katika Siku ya Eid al-Adha, ilhali kondoo ndiye mnyama bora zaidi kuchinjwa endapo anapatikana, akieleza kuwa nyama ya kondoo ni bora na tamu zaidi kuliko ya mbuzi, na kwamba asili ya mnyama wa kuchinjwa katika Eid ni kondoo.

Kuhusu ibada ya Hijja, ameeleza kuwa mahujaji huenda Makkah kuitikia wito wa Mwenyezi Mungu kupitia Nabii Ibrahim (as), na wanaporejea huhesabiwa kama waliotakasika dhambi zao kama siku walizozaliwa.
Hata hivyo, ametoa onyo kuhusu baadhi ya tabia zisizofaa, akisema kuwa baadhi ya watu huingia katika ibada ya Hijja bila maandalizi ya kiroho ya kutosha, na wengine hurejea katika makosa na dhambi zao za awali.

Aidha, amekosoa tabia ya baadhi ya mahujaji, hasa vijana, kutumia ibada ya Hijja kwa kujionesha mitandaoni kupitia picha na “selfie”, akisisitiza kuwa ibada ni kwa ajili ya Mwenyezi Mungu pekee na si kwa ajili ya kuonekana na watu au kutafuta sifa.

Sheikh alihitimisha kwa kusisitiza umuhimu wa kufanya ibada kwa ikhlasi na kuepuka riyaa, akibainisha kuwa malipo ya ibada hutoka kwa Mwenyezi Mungu pekee.

Tags

Your Comment

You are replying to: .
captcha